Simulizi Za Gilbert

Simulizi Za Gilbert

Share

Officialy Page ya Simulizi na Riwaya za mwandishi wako Gilbert Evarist Mushi. WhatsApp +255765824715

15/09/2025

Riwaya ya Kipelelezi: Eva wa Edeni
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone number : 0765824715

Sehemu ya 03
Ni saa mbili na nusu asubuhi, Bi Sandra na Bwana Henry wanapata chai taratibu huku kila mmoja mkono wake mmoja ukichezea simu yake ya mkononi. Bwana Henry yeye alikuwa akifwatilia mubashara kipindi cha mirindimo ya asubuhi kupitia TBConline katika mtandao wa youtube. Mada iliyokuwa ikijadiliwa ni kuhusiana na wimbi la upotevu wa watoto huku mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro ikiongoza.
Kwa upande wake Bi Sandra yeye alikuwa katika uwanja wa meseji akijibishana na mtu. Alikuwa ni mwingi wa hasira huku akichakata ujumbe wa maandishi kwa kasi huku vidole vikitetemeka.

"Madame, kuna mzigo wako umeletwa hapa" Birigitha alisimama pembeni ya bosi wake akiwa amebebelea kiboksi kidogo chenye maua kwa juu.

"Ni nani kakupatia?" Bi Sandra akauliza kwa mshangao huku akiweka simu mezani. Akapokea mzigo ule.

"Ni kijana mwendesha pikipiki, ameniambia yupo nje anakungoja k**a utakuwa na chochote cha kumweleza." Birigitha alijibu.

"Mwambie nakuja" akasema huku akikifungua kiboksi kile.
Looooh! Alikiangusha kiboksi kile chini, kidole kidogo cha mkononi kikatoka ndani ya kiboksi kile kikiwa kimefungwa pamoja na flashi ndogo.
Hakika aliogopa.
Bwana Henry haraka alitoka nje lakini hakumwona mtu yule aliyeleta kiboksi kile, na hapo wakakumbuka kosa walilolifanya hadi kutumiwa kidole cha mtoto wao. Hawakuwa na namna ya kufanya zaidi ya kumpigia Afande Richard. Alimjuza kilichotokea

"Windo letu limefeli, tukutane tulipopaki gari." Afande Richard aliwataarifu polisi wenzake baada ya kupokea simu ya Bwana Henry.
Walielekea hadi nyumbani kwa Bwana Henry na kuwakuta yeye na mwenzie wameketi wakiwa na huzuni nyingi katika nyuso zao. Bwana Henry alimpa ishara Afande Richard aitazame flashi iliyoambatanishwa na kidole kile.
Akaichomeka kwenye runinga iliyokuwa ukutani pale sebuleni, na ndani ya flashi ile kulikuwa na video moja tu. Akaichezesha.

"Na haya ndiyo malipo ya kosa mlilolifanya. Ahsanteni, hadi wakati mwingine." yalikuwa ni maneno kutoka kwa mtu aliyevalia kinyago cha kuificha sura yake asiweze kufahamika. Nyuma ya mtu yule alionekana Kinje anayeugulia maumivu.
Bi Sandra alikuwa akibubujikwa na machozi. Ni nani asiyeujua uchungu wa mama kwa mwanaye? Hakika ilikuwa ni kasheshe.
_____________________

Siku tatu zilipita bila dalili ya watekaji kupiga simu. Afande Richard alijaribu kila namna kutafuta mawasiliano nao kupitia nambari ile waliyoitumia mwanzo lakini hakufanikiwa. Akajaribu hadi kwa wabobezi wa maswala ya kimtandao lakini bado hakufua dafu. Aliikatia tamaa kesi ile.

"Kuna mpelelezi mmoja aitwaye Daniel Mwaseba, nadhani ushawahi kusikia chochote kumhusu. Huyu mpelelezi anatokea idara ya usalama wa taifa, yupo mkoani kwetu kwa ziara maalum ya kitalii yeye na mke wake wakitarajia kuupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea hifadhi ya taifa ya Mkomanzi. Najaribu kufanya jitihada za kuushawishi uongozi wake watusaidie kutupatia huyu mpelelezi asaidiane nawe" Bwana Patrick Ndakidemi ambaye ni mkuu wa kituo cha polisi Kimaroroni, alikuwa akijadiliana na Afande Richard ofisini kwake.
Na kweli yakafanyika mawasiliano kati ya kituo chake cha polisi na idara ya usalama wa taifa makao makuu, akajuzwa kwamba Daniel Mwaseba yupo likizo hivyo k**a ataridhia bila ya shuruti likizo ikavunjwa basi atasaidiwa.

Daniel Mwaseba, kijana mtanashati na kipenzi cha watanzania wengi lakini adui wa watukutu na wasiofuata sheria za nchi. Kijana huyu alikuwa na mkewe Elizabeth Neville ndani ya gari aina ya Toyota Hilux maeneo ya Shanti Town mjini Moshi. Yalikuwa ni majira ya jioni na walikuwa wakitoka katika mgahawa mmoja wakirudi katika hoteli waliyofikia. Siku mbili kabla walifikia Kibo Palace Hotel wakitokea Kimara Dar es Salaam nyumbani kwao baada ya maazimio ya wawili hao punde tu baada ya kupatiwa likizo ya wiki tatu.

Wakiwa ndani ya gari simu yake ilitoa sauti ndogo ikiashiria kuingia kwa taarifa. Akamtaka mkewe amsaidie kuiangalia huku akiitoa mfukoni simu hiyo na kumkabidhi kwani yeye alikuwa bize na usukani wa gari akiendesha.

"Daniel ni ujumbe kutoka kwa Chifu." Elizabeth alisema punde tu baada ya kuufungua ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa mkurugenzi wa idara ya usalama wa taifa.

"Mmh! Anataka nini tena na wamenipa likizo?" Daniel alihamaki huku akizidisha umakini barabarani.

"Anasema ufungue upande wa barua Pepe kuna jambo amekutumia huko" Elizabeth Neville alisema huku akiwasha data na kuelekea katika upande wa barua pepe. Na hapo aliweza kuona taarifa hiyo.
Alimsomea. Yalikuwa ni maombi kwa Daniel kutoka kituo cha polisi cha Kimaroroni. Punde simu kutoka kwa chifu iliita.

"Ipokee, weka sauti ya juu." Daniel alisema.

"Habari yako kijana wangu Daniel," Chifu Abdallah Ntenga ambaye ni mkurugenzi idara ya usalama wa taifa alimsabahi Daniel

"Salama chifu, shkamoo. kuna mpya gani huko?"

"Marhaba Daniel. Bila shaka hiyo barua umeipitia. Ni jukumu lako kuwakubalia ama kuwakatalia maana sisi tunajua kwamba upo likizo hivyo hatuna uwezo wa kukulazimisha. Nikutakie jioni njema"

"Ahsante sana chifu. Jioni njema pia"
Waliagana, simu ikakatwa. Daniel na mkewe wakashauriana kisha wakakubaliana kuelekea huko kituo cha polisi Kimaroroni kuwasikiliza hapo kesho mapema asubuhi.

Ombi kutoka kwa mkuu wake ni amri.

Na kweli palipopambazuka wakajiandaa na kuelekea huko. Wakaik**ata barabara ya Moshi - Arusha wakiwa ndani ya gari yao, walipofika KiboshoRoad wakachepuka kulia kuik**ata barabara ya kibosho na punde baada ya dakika kadhaa wakafika, na huko wakapokelewa na mkuu wa Kituo akiwa sambamba na Afande Richard. Baada ya majadiliano kwa kina Daniel akiwa sambamba na mkewe walikubali kuwasaidia sakata lile. Daniel akaomba kukabidhiwa faili lenye ripoti kamili inayoeleza kwa kina sakata la mauaji ya mwanafunzi Julieth na upotevu wa mwanafunzi Kinje.
Alikabidhiwa, akaipitia, akaridhika. Akawa tayari kwa uchunguzi kwa siku inayofuata mapema asubuhi.

Daniel atafanikiwa kubaini watekaji hao?

Usikose Sehemu ijayo hapahapa 😊

ITAENDELEA

05/09/2025

Riwaya: Anga ya Washenzi
Imeandikwa na Gilbert Evarist Mushi
Phone: 0765824715.

Msimu wa Kwanza.
Sehemu ya 03

Daniel alipigwa na butwaa baada ya kushuhudia mwanaume huyo akiwa bado imara akizidi kumnyonga, mwanaume yule hata hakutetereka kutokana na kupigwa kisogoni na goti lake. Badala yake mwanaume huyo aliinyoosha shingo yake kuelekea kulia kisha kushoto huku mikono ikiendelea kuik**ata shingo. Daniel Mwaseba akizidi kunyongwa alikiri hii aliyokutana nayo ilikuwa ni anga nyeusi, kwa kuwa hakutegemea k**a mwanaume yule angestahimili uzito wa goti lake ambalo laiti likikupata k**a si kifo basi ni kulala usingizi unaofanana na kifo.

Katika mkono wa Daniel Mwaseba, kidoleni kulikuwa na pete ya shaba, pete ambayo aliinunua akiwa mapumzikoni nchini Ujerumani miaka miwili iliyopita, pete hiyo haikuwa pete ya kawaida k**a zilivyo pete nyingine. Pete hiyo ilikuwa ni silaha tosha kwa Daniel, silaha ambayo angeitumia k**a atakuwa katika mazingira magumu ya kutetea uhai wake, mazingira k**a haya anayokumbana nayo hivi sasa. Kwa kutumia kidole gumba aliikandamiza kwa nguvu pete ile aliyovalia katika kidole cha shahada, hapohapo ikajifyatua na sindano nyembamba ikajichomoza katika uso wa pete. Daniel akazikusanya nguvu zake katika mkono wa kulia uliovalia pete ile, akakunja ngumi yake na kuipeleka mara mbili mfululizo katika bega la jamaa. Jamaa aliendelea kumnyonga Daniel kwa sekunde tatu tu, sekunde ya nne jamaa alilegea na kumdondokea Daniel katika kifua chake, hapo Daniel akaanza kupambana kuivuta pumzi kwa fujo kwani ilibakia kidogo tu aende kuisalimu kuzimu.

"K**a isingekuwa hii pete leo ningekufa, inaonekana watu walio nyuma ya hili ni watu waliojipanga vyema" aliwaza Daniel huku akijitahidi kuvuta pumzi kwa shida. Ngumi mbili alizozipiga ziliishindilia pete katika bega na kupelekea sindano ile yenye sumu kumchoma jamaa.

"Sindano ina sumu kali sana, nisipofanya kitu jamaa atanifia hapa na sitapata chochote, hapaswi kufa hadi nijue katumwa na nani" Daniel aliwaza, haraka alitoa kichupa kidogo chenye maji ya rangi ya shaba katika mfuko wa koti lake, akaichana nguo ya jamaa pale begani alipokita pete ile. Aliona alama mbili zilizovimbia kwa matone madogo ya damu, alama ambazo bila shaka ni ile sindano ilipenyeza baada ya kupiga ngumi zile. Daniel akafungua kichupa kile na kudondoshea tone moja la maji yale ambayo yalikuwa ni maalumu kwa kupunguza kasi ya usambaaji wa sumu, kilichobaki ilikuwa ni yeye kumwaisha hospitalini ili kuuokoa uhai wake. Baada ya hapo alichomoa simu yake na kuitafuta namba ya daktari kutoka hospitali ya KCMC, alikuwa ni Dokta Yusha ambaye ni rafiki yake wa muda mrefu.

Dokta Yusha alikuwa akitoka katika chumba cha upasuaji baada ya kudumu huko kwa takribani lisaa limoja, Dokta Yusha alikuwa ni mmoja kati ya madaktari wakubwa na maarufu katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi. Alikuwa akizipiga hatua zake kuelekea katika ofisi yake, ndipo katika mfuko wa koti lake alisikia simu yake ikitoa mtetemo kuashiria kuna mpigaji. Aliitoa na kutazama kwa makini, alipoitazama alimfahamu mpigaji ni nani, akaipokea na kuiweka katika sikio lake la kushoto..

"Dokta Yusha habari? Naomba msaada wako haraka, kuna mtu wa muhimu sana hapa amezidiwa na sumu, ndani ya dakika kumi zijazo atanifia. Ni wa muhimu sana dokta, njoo na vifaa hapa five Star hotel juu ghorofani kabisa" Daniel alisikika simuni, na simu ikakatwa.
Dokta Yusha alielewa. Palepale aliingia katika ofisi yake na kuchukua kibegi chenye baadhi ya vitu ambavyo aliviona vitamsaidia aendapo, bila kubadili vazi lake la kidaktari alielekea nje na kuchukua usafiri wake. Kutoka pale hospitalini hadi ilipo hoteli ilimchukua dakika sita tu kutokana na barabara kutokuwa na foleni yoyote.
*******

Taarifa ya kubadilishwa kwa helikopta ilionekana kumshtua sana jenerali Evance, hakuwa amepata taarifa yoyote kutoka kwa vijana wake tangu awakabidhi kazi ya kuimarisha usalama. Ni jana tu alitoka kuzungumza na vijana wake watatu aliowapendekeza katika kazi ya kuzunguka na helikopta angani, na leo aliona helikopta angani ikizungukazunguka hivyo akaamini ni vijana wake kiasi kwamba hakuwa tena na wazo la kuwasiliana nao.

"Hebu ngoja niwasiliane nao kwanza nijue kulikoni hadi wabadilishe helikopta bila kuniambia" alisema Jenerali Evance ambaye ni mkuu wa majeshi ya Tanzania, palepale alitafuta namba ya kijana mmojawapo kati ya watatu aliowapa kazi hiyo. Alimpigia David. Simu iliita na baada ya sekunde tano ikapokelewa

"David mmefanya kitu gani na wala hamsemi? Kwanini mmebadili helikopta bila kutoa taarifa? Upumbavu gani huu mnafanya kinyume na utaratibu?" jenerali Evance alianza kufoka kwa ghadhabu baada ya simu ile kupokelewa

"Mkuu hata sielewi ni kitu gani kimetokea, tulipoingia ndani ya helikopta ili tuweze kuiwasha ilitokea hali ambayo hata siielewi, mimi na wenzangu wawili tulipitiwa ghalfa na usingizi mkuu, ndio kwanza nimetoka katika usingizi mzito mkuu. Wenzangu bado hawajazinduka, nimejaribu kuwaamsha lakini hawaonyeshi dalili ya kuamka kabisa, nahisi kuna mtu ametuchezea mchezo," David alieleza simuni

"Unasema nini! Ooh shiit..... Ina maana hii helikopta inayoranda angani sio nyie?" Jenerali Evance aliuliza kwa kuhamaki, Upande wa Chifu Abdallah hali haikuwa nzuri hata kidogo. Kitendo cha Evance kuuliza maswali kwa namna ya mshangao alibaini kwa sasa mambo hayapo sawa kabisa, na huu ulikuwa ni mwiba mchungu sana kwake na katika idara yake. Alimsogelea jenerali Evance apate kusikia maongezi yale kwa ukaribu zaidi

"Kuna hatari hapa, hii sehemu si salama kwa Rais wetu. ndio kwanza vijana wangu wanatoka katika usingizi wa kifo baada ya kusinzia ghafla wakati wakijiandaa kupanda helikopta, bila shaka walifanyiwa mchezo walipotaka kuiwasha helikopta" jenerali Evance alimwambia Chifu Abdallah, palepale alipiga hatua kuondoka lakini ghafla alishikwa mkono na Chifu Abdallah.

"Wewe ni mtu imara, hatupaswi kukurupuka katika hili. Tutume vijana wafuatilie ni nani yupo nyuma ya hili, hivi sasa napozungumza na wewe tayari vijana wangu wapo kazini kimyakimya kufuatilia nani ana nia ya kuvuruga ziara hii." aliongea Chifu Abdallah baada ya kumshika jenerali Evance mkono

"Hii ni hatari Bwana Abdallah, endapo likitokea la kutokea hapa sisi ndio tutatazamwa, lazima tufanye kitu" Jenerali Evance akamwambia Chifu Abdallah

"Nawaamini vijana wangu, muda si mrefu watanipa majibu mazuri, wewe tafuta kijana wako mmoja aungane na kijana wangu ili wafuatilie nani amefanya hili hadi hao vijana washindwe kupaisha helikopta angani, na hiyo iliyopo juu angani ifuatiliwe na wahusika wak**atwe"
Maneno ya Chifu Abdallah yakamtuliza Jenerali Evance kwa kiasi fulani, akachukua ushauri ule na palepale akaitoa simu yake kuisaka namba ya kijana wake mwingine anayemtumaini sana.

"Ngoja nimwite kijana wangu yupo hapahapa ziarani, naomba ashirikiane na kijana wako ili zoezi liende haraka. Huyu kijana wangu yeye ni mzuri sana kwa mapambano kuliko upelelezi, ni miongoni mwa wanajeshi waliorudi salama baada ya kumalizika kwa vita nchini Afrika ya Kati, kwa kuwa vijana wako ni hodari katika upelelezi naomba umuunganishe na vijana wako ili nguvu iongezeke, ninamwamini sana" Jenerali Evance anamwambia Chifu kwa unyenyekevu mkubwa.

"Ataambatana na Elizabeth Neville waifuatilie helikopta ile, mtaarifu aje sasa hivi maana mambo yanaweza kuharibika k**a tutazidi kuchelewa"
Palepale Jenerali Evance anampigia Gilbert Mwaitika, ambaye ni mmoja kati ya wanajeshi hodari sana katika vita. Gilbert Mwaitika ni mtaalamu wa mapambano ya ana kwa ana, ya kutumia silaha, na hata ya mbinu za kikomandoo. Miaka kadhaa iliyopita mwanajeshi huyu alishiriki vyema katika misheni iliyoitwa Biashara ya Watoto, iliyoandikwa katika majarida na mwandishi mmoja, katika misheni hiyo mwanajeshi huyu alionyesha ukomavu wa hali ya juu katika kupambana na watu waliokuwa wakifanya biashara hiyo, jambo lililompelekea apande chati kutoka upolisi hadi kuwa mwanajeshi komandoo baada ya kwenda mafunzoni nchini Iraq. Na huko ndipo alipokamilika na kuwa komando.
Jenerali Evance alimpatia maelekezo Gilbert Mwaitika ni wapi alipo ili aje. Wakati huo chifu naye alimfuata Elizabeth Neville na kumpatia kazi mpya.

"Unaona pale aliposimama mkuu wa majeshi, Jenerali Evance? hebu nenda mfuate sasa hivi, kuna kijana atakuunganisha nae ili mfuatilie ile helikopta inayoranda angani" Chifu alimwambia Elizabeth Neville.
ITAENDELEA

Kina Daniel watafanikiwa kujua chochote? Vipi kuhusu Helikopta inayoranda angani Elizabeth Neville na Gilbert Mwaitika watafanikiwa kuinasa? Ungana nami katika sehemu ijayo hapahapa. Riwaya hii ina Jumla ya Misimu Mitano. Msimu wa Kwanza sasa upo tayari, Ni kwa Tshs 1000 tu unaweza kuupata. Lipa kwenda M pesa namba 0765824715 kisha njoo WhatsApp kwa namba 0765824715 nikutumie. Ukilipia 3000 utapata riwaya yote.

Want your public figure to be the top-listed Public Figure in Moshi?
Click here to claim your Sponsored Listing.

Category

Telephone

Address

Moshi