Wasafi FM

Wasafi FM

Share

The leading radio station in Tanzania specializing in the latest music & entertainment news.

12/06/2026

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema ameridhishwa na maandalizi ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu k**a SabaSaba, yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28 mwaka huu, huku akitoa wito kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho hayo ya kihistoria yanayotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Mapunda alitoa kauli hiyo Juni 12 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika viwanja vya maonesho, ambapo amesema maandalizi yanaendelea vizuri na yanaendana na hadhi ya maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya Sabasaba.

Amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa ya kipekee kwa kuwa yatatoa fursa kwa wananchi kujionea maendeleo katika sekta za biashara, uwekezaji na utalii, sambamba na kusherehekea historia ya maonesho hayo ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo.

Aidha, Mapunda amezitaka taasisi na ofisi zote za Serikali kuhakikisha mabanda yao yanakamilika ifikapo Juni 20 ili wageni na washiriki watakaofika kwenye maonesho hayo washuhudie maandalizi bora yanayoakisi hadhi ya maadhimisho hayo muhimu.

Kwa upande wake, Dkt Latifa Khamis Mkurugenzi Mkuu wa TANTARADE amesema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha maonesho ya mwaka huu yanakuwa makubwa na ya aina yake kwa kutoa fursa za biashara, uwekezaji, burudani na kujifunza kwa wananchi, wazalendo na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Amesema hadi sasa nchi 23 zimethibitisha ushiriki wao katika maonesho hayo, huku makampuni 256 ya kimataifa yakionesha nia ya kushiriki na zaidi ya makampuni 2,776 ya ndani yakijiandikisha kushiriki, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani na fursa za kibiashara kwa washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Aidha, maonesho hayo yatapambwa na programu mbalimbali zikiwemo “Usiku wa Kash Kash”, matembezi maalumu ya kuhamasisha matumizi ya bidhaa za Made in Tanzania pamoja na hafla ya Golden Jubilee itakayofanyika Julai 7 kwa ajili ya kutambua na kuwatunuku wadau waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Maonesho ya Sabasaba kwa kipindi cha miaka 50.

12/06/2026

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeomba kuendelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ireland kupitia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Maziwa Faida kuanzia mwaka 2027 hadi 2032, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuongeza uzalishaji wa maziwa, kuboresha tija na kuinua maisha ya wafugaji nchini.

Ombi hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Madele, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Ubunifu na Teknolojia katika Sekta ya Maziwa (TALIRI Open Day 2026) yaliyofanyika katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) Kanda ya Mashariki, jijini Tanga.

Dkt. Madele alisema Mradi wa Maziwa Faida unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania kupitia TALIRI na Taasisi ya Maendeleo ya Kilimo na Chakula ya Ireland (TEAGASC), kwa ufadhili wa Serikali ya Ireland kupitia Ubalozi wake nchini Tanzania, umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya maziwa, hasa Mkoa wa Tanga.

Alieleza kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, wafugaji wengi walikuwa wakizalisha wastani wa lita tatu hadi tano za maziwa kwa ng’ombe mmoja kwa siku. Hata hivyo, kupitia matumizi ya teknolojia bora za ufugaji, malisho ya kisasa, huduma za ugani zilizoimarishwa pamoja na mafunzo kwa wafugaji, uzalishaji umeongezeka hadi wastani wa lita 15 kwa ng’ombe mmoja kwa siku katika maeneo mengi yaliyofikiwa na mradi.

“Matokeo haya yanaonesha wazi mchango mkubwa wa utafiti, ubunifu na ushirikiano wa kimataifa katika kuongeza tija, kuboresha kipato cha wafugaji na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini,” alisema Dkt. Madele.

Aidha, alisema Tanzania kwa sasa inazalisha takribani lita bilioni 4.1 za maziwa kwa mwaka huku mahitaji ya taifa yakikadiriwa kufikia lita bilioni 13 kwa mwaka, hali inayoashiria uwepo wa fursa kubwa ya kuwekeza zaidi katika sekta ya maziwa ili kupunguza pengo la uzalishaji na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Suzanne Keatinge, aliipongeza TALIRI kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo na kuwatambua watafiti, maafisa ugani pamoja na wadau mbalimbali waliochangia mafanikio yake.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TALIRI, Prof. Erick Komba, aliishukuru Serikali ya Ireland kwa ufadhili wake na kueleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maziwa Faida (2021/2022–2025/2026) yameweka msingi imara wa kuendelea kuleta mageuzi chanya katika sekta ya maziwa nchini.

Prof. Komba alisema TALIRI itaendelea kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti, ubunifu na teknolojia zilizozalishwa kupitia mradi huo zinawafikia wafugaji wengi zaidi ili kuongeza uzalishaji, tija na ushindani wa sekta ya maziwa.

Aliongeza kuwa mradi huo uliogharimu zaidi ya Euro milioni 3, sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 7 za Kitanzania, umenufaisha zaidi ya wanawake na vijana 3,000 katika ukanda wa pwani ya mashariki, hususan Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Kwa mujibu wa Prof. Komba, mafanikio mengine ya mradi huo ni pamoja na kufanya tafiti za malisho bora yanayostahimili mazingira ya ukanda wa pwani, kubaini aina bora za ng’ombe wa maziwa, kuwajengea uwezo maafisa ugani, kutoa mafunzo kwa wafugaji, kuimarisha vyama vya ushirika vya wafugaji, kuboresha miundombinu ya utafiti na kuanzisha mashamba darasa yanayotumika kusambaza teknolojia za kisasa za ufugaji.

Mradi wa Maziwa Faida umetajwa kuwa mfano wa mafanikio wa ushirikiano wa maendeleo unaochochea matumizi ya utafiti, ubunifu na teknolojia katika kutatua changamoto za uzalishaji wa maziwa na kuchangia ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo nchini Tanzania.

Want your business to be the top-listed Media Company in Dar es Salaam?
Click here to claim your Sponsored Listing.

Category

Address


Mbezi Beach
Dar Es Salaam